Senegal: Serikali inasema inachukua hatua kudumisha amani na utulivu
Nairobi – Wizara ya mambo ya ndani nchini Senegal, imesema inachukua hatua kuhakikisha kuna utulivu na amani kwenye taifa hilo haswa wakati huu maandamano ya upinzani yakiendelea kushuhudiwa katika baadhi ya sehemu za taifa hilo.
Imechapishwa:
Maandamano bado yanashuhudiwa katika mji mkuu Dakar, na Ziguinchor, eneo ambako kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko ni meya.
Hatua ya kukamatwa kwa Sonko na kufutwa kwa chama chake cha kisiasa wikendi iliyopita imeaamsha maandamano mapya.
Sonko ambaye anazuiliwa na polisi, ametangaza kuaanza mgomo wa kususia chakula akiwa gerezani.
Siku ya Jumatatu waziri wa mambo ya ndani nchini humo Antoine Félix Abdoulaye Diome, alitangaza kwamba serikali imefuta chama cha (Pastef) chake Sonko kwa tuhuma za kuchochea vurugu zilizoshuhudiwa jijini Dakar mwezi uliopita.
Video kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha waandamanaji wakiwarusha maofisa wa usalama mawe kufutia hatua hiyo ya kukatwa kwa kiongozi wao na kuvunjwa kwa chama chake.
Hii ni mara ya tatu chama cha kisiasa kinavunjwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi tangu kujipatia uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka wa 1960.
Wafuasi wa Pastef wamemtuhumu rais wa Macky Sall na chama chake tawala kwa kujaribu kumfungia nje mpinzani wake ambaye pia aliibuka wa tatu katika uchaguzi wa urais wa 2019.