Pata taarifa kuu
SOMALIA-KENYA

Somalia yaituhumu Kenya kujaribu kutatiza usalama wake

Waziri wa habari wa Somalia, Osman Abukar Dubbe, ameituhumu nchi ya Kenya, kwa kujaribu kuzorotesha hali ya usalama kwenye taifa lake, wakati huu likijiandaa kwa uchaguzi wa wabunge na rais.

Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed.
Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed. Yasuyoshi CHIBA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Katika mahojiano na kituo cha televisheni ya taifa ya Somalia, waziri Dubbe, amesema “Tunaiheshimu Kenya, tunaheshimu ushirikiano na maelewano tuliyonayo. Kwetu sisi tumeheshimu hiyo misingi. Hata hivyo, Kenya inaonekana haina nia badala yake inataka kuchukua uelekeo wa kutaka kuchukua bahari na ardhi yetu.”

 

Waziri huyo ameituhumu Kenya kwa kuingilia siasa zake pamoja na kutoa hifadhi kwa viongozi wa upinzani jijini Nairobi.

 

Wanasiasa kutoka Somalia ambao wengi wanatokea kwenye eneo la Jubabaland ni miongoni mwa wale walioripotiwa kufanya vikao jijini Nairobi kuhuu uchaguzi wa taifa hilo wa mwaka 2020/2021.

 

“Utawala wa Mogadishu haujawahi kutoa hifadhi kwa mwanasiasa hata mmoja wa Kenya, ambaye anataka kutengeneza mzozo kwa majirani, lakini badala yake, Nairobi imekuwa kitovu mashambulizi dhidi ya Somalia. Imekuwa ni kitovu cha kuharibu makubaliano ambayo yanafikiwa ndani ya Somalia.” alisema waziri huyo.

 

Dubbe pia amesema wapiganaji wa Al Shabaab, wamefanikiwa kuchukua mji mmoja wa kusini mwa nchi hiyo, baada ya wanajeshi wa Kenya ambao ni sehemu ya vikosi vya kulinda amani AMISOM, waliamua kuondoka.

 

“Baada ya wanajeshi wa Kenya kuondoka kwenye maeneo hayo bila ya kutoa taarifa kwa yeyote, yalichukuliwa na wanamgambo wa Al Shabaab. Hebu fikiria madhila ambayo raia wa Somalia wanapitia hasa wanaokaa kwenye hayo maeneo. Je hilo ni jambo tunaweza lipuuza. Nenda kawaulize wakazi wa mji wa Fahfadhun, kile wamepitia.” alisema waziri Dubbe.

 

Tarahe 30 ya mwezi uliopita, Serikali ya Mogadishu ilimuita nyumbani balozi wake jijini Nairobi pamoja na kumuitisha kwa majadiliano balozi wa Kenya mjini Mogadishu.

 

Kwa upande wake Serikali ya Kenya kupitia kwa wizara ya mambo ya njem imekanusha kuingilia masuala ya ndani ya Somalia.

 

Uhusinao baina ya Kenya na Somalia, umekuwa si wa kuridhisha katika siku za hivi karibuni, kwa sehemu kubwa ukichangiwa na mvutano wao wa umiliki wa eneo la bahari lenye ukubwa wa kilo;eta za mraba laki 1 na elfu 50, ambapo kila upande umekuwa ukidai ni sehemu yake hadi kupelekana katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa mizozo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.