Pata taarifa kuu
COTE D'IVOIRE-SORO-SIASA-USALAMA

Cote d'Ivoire yajiondoa kwenye mkataba unaounda Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu

Nchi ya Cote d'Ivoire imetangaza kujiondoa kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu kwa kile inachosema kuwa haina imani na Mahakama hiyo.

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao yake Arusha, Tanzania.
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao yake Arusha, Tanzania. ©Cour africaine
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja baada ya Mahakama hiyo yenye makao yake mjini Arusha, nchini Tanzania, kufuta hati ya kukamatwa kwa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Guillaume Soro na kuamuru kuachiliwa huru kwa wafausi wake 19.

Cote d'Ivoire imechukua hatua hii baada ya kumhukumu jela miaka 20 Bwana Soro ambaye anaishi nchini Ufransa kwa kosa la kutumia fedha za umma, kujenga nyumba ya kifahari jijini Abidjan.

Guillaume Soro ambaye yuko ukimbizini nchini Ufaransa, hakuwepo wakati hukumu hiyo ilipotolewa na mahakama ya Abidjan Jumanne wiki hii.

Guillaume Soro na wanasheria wake wanasema hukumu hiyo ilitolewa na mahakama baada ya kushinikizwa ili kumzuia kuwania nyadhifa ya uongozi nchini humo.

Hivi karibuni Guillaume Soro alitangaza kuwania katika uchaguzi wa urais ujao nchini humo uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Soro anashtumiwa kwamba alitumia fedha za umma takriban Euro Milioni Saba kujinunulia makaazi ya kifahari jijni Abidjan mwaka 2007 alipokuwa waziri mkuu.

Hata hivyo washirika wake wa karibu ikiwa ni pamoja na ndugu zake, wabunge na wafuasi wake wanaendelea kuzuiliwa nchini Cote d'Ivoire baada ya kukamatwa tangu mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana.

Kulingana na wanasheria wao, kesi hii ni ya kisiasa na ilianza kwa sababu Guillaume Soro, mshirika wa zamani wa Alassane Ouattara, aliachana naye na kutangaza kuwania katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.