Pata taarifa kuu
DRC

DRC: Vyama vya upinzani katika kampeni ya kumuondoa Kabila

Makundi kadhaa ya vyama vya upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, yametangaza kuanzisha kampeni ya kushinikiza Rais Joseph Kabila aondoke madarakani, wakati muhula wake utakapotamatika, Desemba 20 mwaka huu.

Kiongozi wa upinzani na mgombea urais DRC, Moise Katumbi.
Kiongozi wa upinzani na mgombea urais DRC, Moise Katumbi. REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Kampeni hiyo iliyopewa jina "Bye-Bye Kabila" yaani kwaheri Kabila, inataka Rais Kabila, ambaye anatuhumiwa na upinzani kwa kuchelewesha kwa makusudi kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini humo, aondoke madarakani kwa hiari bila ya masharti.

Marveille Gozo, mmoja wa waandaaji wa kampeni hiyo, amewaambia wanahabari jijini Kinshasa jana kuwa, muungano wao umekusanyika kuufahamisha uma wa watu wa DRC na Jumuiya ya Kimataifa kuhusu kuanza kwa kampeni yao.

Maandamano ya amani ya nchi nzima yamepangwa kufanyika Ijumaa ya wiki hii kwenye miji mbalimbali nchini humo, huku waandaaji hao wakisisitiza kuwa wakati umefika kwa Rais Kabila kuondoka.

Wito huu wa maandamano pamoja na kuanza kwa kampeni ya kushinikiza Rais Kabila kuondoka madarakani, inakuja wakati huu ambapo Serikali imepiga marufuku kufanyika kwa maandamano yoyote nchini humo.

Juma lililopita, polisi mjini Kinshasa, walimzuia nyumbani kwake, rais wa chama cha UDPS, Etienne Tshisekedi, ambaye alikuwa ameitisha maandamano ya nchi nzima kushinikiza Rais Kabila kuondoka madarakani.

Rais Kabila aliingia madarakani baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent-Desire Kabila, aliyeuawa na mlinzi wake mwaka 2001, wakati wa vita ya pili ya Congo, ambayo ilimalizika miaka miwili baadae.

Akichaguliwa mwaka 2006, alifanikiwa kushinda muhula wa pili wa kipindi cha miaka mitano mwaka 2011, katika uchaguzi ambao upinzani ulidai umeshinda, huku waangalizi wa kimataifa wakikiri kuwa ulikuwa na kasoro nyingi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.