Pata taarifa kuu
TANZANIA-TGNP

Tanzania: TGNP yataka rais kuzingatia usawa wa kijinsia wakati wa uteuzi wa viongozi wa Serikali

Mtandao wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi kwa uratibu wa Mtandao wa jinsia, TGNP, umetoa rai kwa Serikali kuzingatia usawa wa kijinsia wakati wa uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi.

Mkurugenzi wa mtandao wa Jinsia, TGNP, Lilian Liundi akizungumza na vyombo vya habari
Mkurugenzi wa mtandao wa Jinsia, TGNP, Lilian Liundi akizungumza na vyombo vya habari RFI
Matangazo ya kibiashara

Mtandao huo mbali na kupongeza jitihada za Serikali ya rais John Pombe Magufuli za kurejesha utawala wa bora na kuwa na safu ya viongozi waadilifu, umedai kuingiwa hofu kuhusu dhamira ya kutambua nguvu kubwa za wanawake katika kuwezesha jitihada za awamu ya tano hasa katika kuleta mabadiliko katika maisha ya Watanzania, wanawake kwa wanaume.

Mtandao wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi umeongeza kuwa umekuwa ukifuatilia kwa ukaribu uteuzi wa viongozi katika nafasi mbalimabli za kimaamuzi serikalini ikiwa ni pamoja na uteuzi wa Makatibu Wakuu, Mawaziri na Wakuu wa Idara/Taasisi mbalimbali uliofanywa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Umeongeza kuwa, katika uteuzi huo jumla ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu walioteuliwa ni 50 idadi ambayo ni pungufu kidogo ikilinganishwa na mwaka 2014 ambako jumla yao ilikuwa 53, ambapo idadi ya Makatibu Wakuu imeongezeka kutoka 23 mwaka 2014 hadi 29 wakati Manaibu Katibu Wakuu imepungua kutoka 30 mwaka 2014 hadi 21 mwaka huu, na kwamba kati ya nafasi zote 50 za walioteuliwa na Rais, wanawake ni 10 pekee ambayo ni sawa na asilimia 20.

Kwenye taarifa ya mtandao huo wa wanawake, imeongeza kuwa kwa tathmini waliyoifanya, idadi ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu wanawake imepungua kwa kiasi kikubwa.

Takwimu za mwaka 2014 zinaonesha kuwa, idadi ya wanawake waliokuwa Makatibu wakuu au manaibu katibu wakuu ilikuwa 20 sawa na asilimia 37.7 huku wanaume wakiwa 33 sawa na asilimia 62.3, ambapo katika uteuzi uliofanyika mwaka huu, jumla ya wanawake makatibu wakuu na manaibu ni 10 sawa na asililimia 20 tu huku asilimia 80 inayobakia ikishikiliwa na wanaume.

Taarifa yao imeongeza kuwa kwa kuzingatia takwimu hizo, ni dhahiri kuwa, idadi ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu wanawake imepungua kutoka asilimilia 37.7 mwaka 2014 hadi asilimia 20 mwaka 2015, ikiwa ni tofauti ya asilimia 17.7 ambayo ni kubwa na hivyo kuongeza pengo la jinsia katika nafasi za kufanya maamuzi.

Wanaharakati wa masuala ya jinsia wameeleza kushtushwa na uteuzi huo kwa kile wanachodai kuwa walitarajia kuona uteuzi wa rais unazingatia usawa wa kijinsia uliofanyika katika nafasi za juu za Serilikali (Rais na Makamu wake) na kwamba teuzi za nafasi za uongozi zingezingatia usawa wa kijinsia kama suala la msingi hasa katika kuhakikisha kuwa wanawake na makundi mengine wanashiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi.

Tanzania kupitia (Tanzania Development Vision 2025) imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na jamii yenye muono wa kimaendelea ambapo pamoja na mambo mengine unakuwa na tamaduni wezeshi hususani kwa wanawake na makundi mengine.

Mtandao wa jinsia umetoa rai kwa Rais na viongozi wote kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa na Tanzania hususani ile inayohusu usawa wa kijinsia ili kupunguza pengo lililopo kuelekea usawa wa 50/50 katika nafasi za uongozi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.