Pata taarifa kuu
KENYA

Waziri wa Usalama nchini Kenya ashinikizwa kujiuzulu

Baada ya shambulizi la kigaidi lililotekelezwa na kundi la kigaidi la Al Shabab lenye makao yake nchini Somalia mjini Mpeketoni Pwani ya Kenya Jumapili iliyopita na kusababisha vifo vya watu 48, shinikizo sasa zinatolewa kwa Waziri wa Mambo ya ndani nchini humo Joseph Ole Lenku kujiuzulu.Aliyekuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa muungano wa upinzani CORD Raila Odinga amesema mashambulizi ya Mpeketoni yamedhihirisha wazi kuwa Waziri huyo ameshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ya kuhakikisha usalama raia wa nchi hiyo.

Magari yaliyoteketezwa kwa moto na kundi la Al Shabab hapo Mpeketoni Kenya
Magari yaliyoteketezwa kwa moto na kundi la Al Shabab hapo Mpeketoni Kenya STANDARD News
Matangazo ya kibiashara

Shinikizo kama hizo pia zinatolewa na tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu nchini humo, ambayo imesema ni sharti Waziri huyo awajibike kwa kushindwa kulinda maisha ya wakenya.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Nairobi, Waziri Ole Lenku alidai kuwa kuna uwezekano kuwa mashambulizi hayo yalichochewa kisiasa kutokana na mikutano ya kisiasa ya muungano wa upinzani CORD inayoendelea kuishinikiza serikali kukubalia mazungumzo ya kitaifa kuzungumzia maswala tata nchini humo likiwemo la usalama.

Jeshi la Polisi linaendeleza Operesheni ya angani na ardhini huko Mpeketoni kuwasaka wanamgambo hao wa Al Shabab ambao hawajulikani waliko.

Wachambuzi wa maswala ya usalama wanaendelea kusisitiza kuwa Kenya inakabiliwa na changamoto katika mtandao wake wa usalama na utekelezaji wa habari muhimu kuhusu maswala ya usalama nchini humo.

Francis Onditi mtaalam wa usalama akiwa Nairobi nchini Kenya ameiambia RFI Kiswahili kuwa, mashambulizi nchini Kenya yataendelea kushuhudiwa ikiwa idara ya usalama nchini humo haitafanyiwa marekebisho muhimu.

'Kenya inakabiliwa na mashambulizi haya kwa sababu mfumo wake wa Inteljensia umetikisika, serikali inastahili kuthathmini upya sera yake kuhusu ukusanyaji, na utekelezaji wa habari muhimu kuhusu usalama” Onditi amesisitiza.

Aidha amesema kuwa “ Kenya imetekeleza kutokana na kutokuwa na sera thabiti kuhusu uhamiaji, kuna wageni wengi ambao hawajafahamika wanafanya nini nchini”.

Kundi la Al Shabab linasema linalipiza kisasi kwa kutekeleza mauaji nchini Kenya kwa sababu jeshi la nchi hiyo limeendelea kuwaua Wasomalia katika operesheni ya linda nchi tangu mwaka 2011.

Mashambulizi ya Mpeketoni ndio mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya tangu mwaka uliopita, wakati kundi hilo lilipotekeleza shambulizi katika jengo la biashara la Westage na kusabisha vifo vya watu 67.

Mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, yamewataka raia wake kuwa makini wanapozuru nchini Kenya na tayari Uingereza imewaondoa watalii wake mjini Mombasa kwa hofu ya usalama.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.