Pata taarifa kuu
MALI-MAREKANI-BURKINA FASO

Katibu Mkuu wa UN ataka Makundi ya Wapiganaji wa Kiislam nchini Mali yawekewe vikwazo kutokana na kushirikiana na Makundi ya Kigaidi Duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja huo kuweka vikwazo dhidi ya Makundi ya Kiislam ambayo yanatuhumiwa kutekeleza vitendo vya kigaidi nchini Mali.

Wapiganaji wa Kundi la Waislam wenye Msimamo Mkali wa Ansar Dine ambao wanaendelea kushikilia eneo la Kaskazini mwa Mali
Wapiganaji wa Kundi la Waislam wenye Msimamo Mkali wa Ansar Dine ambao wanaendelea kushikilia eneo la Kaskazini mwa Mali REUTERS/Adama Diarra
Matangazo ya kibiashara

Ban amesema kuwa vikwazo hivyo vinastahili kuwekwa kutokana na Makundi yaliyojitangazia uhuru wa Kaskazini mwa nchi hiyo kuwa na uhusiano na Makundi mengine ya kigaidi Duniani.

Katibu Mkuu wa UN amesema ni vyema nchi wanachama wa kudumu kumi na tano za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zichukulie suala hili kwa uzito wake na hivyo kuweka vikwazo ili kudhibiti madhara ambayo yanaweza kutokea.

Ban licha ya kutaka kuwekwa kwa vikwazo hivyo kwa makundi hayo ambayo yamechukua utawala wa eneo la Kaskazini lakini pia ametoa wito kwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS na Umoja wa Afrika AU kuhakikisha wanapeleka kikosi cha kulinda amani.

Katibu Mkuu Ban ametolea mfano wa Kundi la Ansar Dine kama moja ya watu ambao wamefanya vitendo hivyo vya kigaidi kutokana na kufanya uharibifu hata wa urithi wa taifa hilo ikiwemo makaburi yaliyopo Timbuktu.

Naye Mkuu wa Tume ya Masuala ya Siasa, Amani na Usalama kutoka ECOWAS Salamatu Hassaini Suleiman anasema huu ni wakati muafaka kwa serikali ya mpito kufanyakazi kwa vitendo ili kupata suluhu badala ya kuendelea kutupa lawama kwa Makundi ya Wapiganaji wa Kiislam.

Salamatu amesema vitendo vya kigaidi ambavyo vinafanywa Kaskazini mwa Mali vipo wazi kabisa hivyo ni jukumu la serikali ya mpito kuangalia ni kwa namna gani itarejesha utulivu katika taifa hilo.

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa UN Gerrard Araud ameendelea kusisitiza ECOWAS haina mamlaka ya kupeleka Jeshi nchini Mali kama ambavyo imekuwa ikisema na kueleza serikalu ya mpito.

Balozi Araud anakwenda mbali zaidi na kusema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ndiyo pekee lenye jukumu hilo la kuamua kama kutakuwa na umuhimu wa kupelekwa Jeshi nchini Mali kulinda usalama.

Naye Mpatanishi wa Mgogoro wa Mali kutoka ECOWAS ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso Djibril Bassole anaendelea kukutana na Viongozi wa Kundi la Ansar dine kwa lengo la kupata suluhu na amewasihi wasitishe uhusiano wao na Makundi ya Kigaidi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.