Pata taarifa kuu
MISRI

Maelfu ya wananchi waandamana nchini Misri kupinga unyanyasaji wa wanawake

Maelfu wa wananchi wa Misri wamevamia mitaa mbalimbali ya Mji Mkuu Cairo wakifanya maandamano yakupinga unyanyasaji na kupigwa wanawake ambao waliandamana kushinikiza kuondoka madarakani kwa Utawala wa Kijeshi.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo yalifanyika kuanzia siku ya ijumaa kwenye eneo la Viunga vya Tahrir ambapo maelfu ya wananchi kuzingira jengo la bunge wakitaka utawala wa kijeshi ufikie kikomo.

Wanaharakati nchini Misri ndiyo ambao wameitisha maandamano hayo kupinga vitendo vya askari kuwapiga wanawake ambao walijitokeza kwenye maandamano ya siku tano kushinikiza utawala wa kijeshi ukae kando.

Maandamano hayo yalikuja baada ya kuoneshwa kwa video zikionesha namna ambavyo askari walivyokuwa wakimpiga mwanamke mmoja aliyejitokeza kwenye Viunga vya Tahrir kujumuika na waandamanaji wengine.

Wanaharakati hao wamepaza sauti zao na kutaka Jumuiya ya Kimataifa kuwasaidia katika kufanikisha kuondoka madarakani kwa serikali ya kijeshi sambamba na kusitishwa kwa vitendo vya unyanyasaji wa haki za waandamanaji.

Wanaharakati wa Haki za Wanawake wamekuwa mbogo na kuituhumu wazi wazi serikali ya kijeshi chini ya Field Marshal Mohammed Hussein Tantawi ya kwamba imekuwa ikikandamiza na kukiuka haki za wanawake.

Serikali ya Field Marshal Tantawi imeendelea kujikuta kwenye shinikizo la kutakiwa kuondoka madarakani licha ya yenyewe kushikiria msimamo wa kuendelea kuhudumu hadi pale uchaguzi mkuu uatakapofanyika hapo mwakani.

Maandamano yaliyaotishwa mwishoni mwa juma nchini Misri yameshuhudia watu kumi na wanne wakipoteza maisha huku wengine zaidi ya mia tisa wakijeruhiwa kwenye mapambano baina ya waandamanaji na askari.

Tangu kuanguka kwa utawala wa Rais Hosni Mubarak mapema mwaka huu nchi ya Misri imeendelea kushuhudia maandamano ya kudai mabadiliko na kupinga viongozi ambao walihudumu wakati wa utawala wa Kiongozi huyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.