Pata taarifa kuu
SOMALIA

Uchaguzi nchini Somalia wasogezwa mbele kwa mwaka mmoja zaidi

Baada ya kuwepo mvutano mkubwa ndani ya serikali ya Somalia baina ya wafadhili wa nchi hiyo na viongozi wa upinzani, hatimaye sasa rais wa nchi hiyo Sheikh Sharif Ahmed na Spika wa bunge Sharif Hassan Sheikh Aden wamekubaliana kusogeza mbele uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Rais wa Somali Sheikh Sharif Ahmed alipokutana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Rais wa Somali Sheikh Sharif Ahmed alipokutana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon © Reuters
Matangazo ya kibiashara

Uchaguzi mkuu nchini humo ulipangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu lakini kulijitokeza tofauti baina ya rais na spika wa bunge kuhusiana na tarehe rasmi ya uchaguzi huku Umoja wa Matiafa ukisistiza uchaguzi kufanyika mwaka huu.

Katika mkutano uliowakutanisha viongozi hao mjini Kampala mnamo mwezi uliopita, Spika wa bunge la Somalia Sheikh Aden alipendekeza nchi hiyo kuahirisha uchaguzi mkuu kwa kile alichoeleza kuwa bado hali ya usalama haijatengamaa nchini humo hatua ilyoungwa mkono na rais wa Uganda Yoweri Museven.

Makubaliano hayo mapya sasa yanaashiria kuwa rais Sheikh Sharif Ahmed na Spika wa bunge Sharif Hassan Sheikh wataendelea kubakia kama viongozi wa nchi hiyo mpaka tarehe 20 mwezi wa 8 mwaka 2012 uchaguzi mkuu utakapoitishwa.

Katika hatua nyingine viongozi hao kwa pamoja wamekubaliana kumfuta kazi waziri mkuu wa nchi hiyo kwa kile viongozi hao walichoeleza kuwa waziri mkuu huyo alikuwa mstari wa mbele kuchochea maandamano katika mji wa Mogadishu kupinga uchaguzi kusogezwa mbele.

Nchi hiyo ilijikuta katika maandamano makubwa katika mji wa Mogadishu ambapo baadhi ya wananchi walioandamana walisema kuwa waziri mkuu Mohamed Abdullahi Farmajo ndie kiongozi pekee anaefanya juhudi za kuhakikisha nchi hiyo inarejea katika hali ya amani kwa kuharakisha kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa makubaliano yao ni kuwa waziri mkuu mpya atatangazwa baada ya siku 30 kupita ambapo viongozi hao tayari watakuwa wamepata jina la kupendekeza kuteua waziri mkuu mpya.

Juma lililopita serikali ya Uganda kupitia kwa rais Museven ilitishia kuviondoa vikosi vyake vya kulinda amani nchini humo endapo viongozi wa Somalia wangelazimisha uchaguzi mkuu kufanyika mwaka huu akidai kuwa kufanya uchaguzi mkuu mwaka huu kungewapa nguvu zaidi wapiganaji wa Al-Shaab kupata nguvu zaidi.

Rais Museven katika taarifa yake alisema kuwa kuruhusu uchaguzi mkuu kufanyika mwaka huu kutatoa mwanya kwa wapiganaji kuanza kujikusanya upya na kufanya mashambulizi ambayo yangejaribu uchaguzi mkuu, badala yake akataka kuongezwa kwa muda zaidi ili wanajeshi wa umoja wa Afrika kwa kushirikiana na vikosi vya serikali waendelee kutwaa miji zaidi toka kwa waasi.

Wakati hayo yakiendelea mapambano baina ya vikosi vya AMISON vya umoja wa Afrika vimeendelea na mashambulizi zaidi dhidi ya wapiganaji wa Al-Shaabab ambapo wameendelea kutwaa miji iliyokuwa inakaliwa na wapiganaji hao.

Hata hivyo taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa wapiganaji wanaoipinga serikali ya nchi hiyo bado wameendelea kushikilia maeneo mengi ya kusini mwa nchi hiyo ambapo ndiko wamekuwa wakianzia mashambulizi yao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.