Pata taarifa kuu
Misri

Nchini Misri wapinzani wasioridhika warejea barabarani.

Wanaharakati wa Misri wametowa wito Ijumaa, Mei 27, 2011 Kuanzisha "mapinduzi ya pili" mchana wa Ijumaa wanaharakati hao walikusanyika katika eneo la Tahrir mjini Cairo. Wengi wao hawakuridhishwa kiasi kikubwa na maendeleo ya nchi yao tangu kupinduliwa kwa serikali ya Mubarak, Februari 11, wanaharakati hao wanataka kueleza hadharani hasira zao kuhusu hatua zisizoridhisha zinazochukuliwa  katika mchakato wa  kukuza demokrasia.

Waandamanaji  Tahrir Misri
Waandamanaji Tahrir Misri REUTERS/Amr Abdallah Dalsh
Matangazo ya kibiashara

Lengo lilikuwa kuweka wazi maumivu yote walionayo kuhusu utawala wa Baraza Kuu la vikosi vya jeshi (AFSC), linalotawala nchini humo. Baadhi ya wanablogu 375 wameitikia wito wa maandamano ya Ijumaa. Jumuiya ya  Umoja wa Vijana kwa ajili ya mapinduzi ya Aprili 6 ilitoa wito kupitia mtandao wa kijamii wa  Facebook, wa kuwataka Wamisri kuteremka barabarani hasa kwenye viwanja  maarufu vya Tahrir katikati mwa mji mkuu Cairo na "kukomesha ufisadi wa kisiasa." Maelfu ya wanachama wa mitandao ya kijamii walithibitisha mapema kushiriki katika maandamano hayo.

 
Harakati hizo mbili za maandamano ya leo ndizo zilizokuwa kwenye safa ya mwanzo katika maandamano ya Januari na Februari yaliopelekea Rais Hosni Mubarak kuachia ngazi. wanaharakati hao pia walihudhuria mkutano wa Kitaifa , na kujiondoa baadae wakikishutumu chama cha Rais wa zamani Hosni Mubarak kutumia jukwaa hilo la mkutano wa kitaifa ili kurejea tena katika mstari wa mbele wa kisiasa.

 
Kundi la Muslim Brotherhood lilikataa kujiunga na maandamano hayo. Kundi hilo limeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu wito wa  maadanamano usiokoma. Katika taarifa yake, harakati inayoongozwa na Mohamed Badie imetahadharisha juu ya jaribio lolote la mgawanyiko kati ya raia na jeshi. Jeshi la Misri limeamuwa kukaa mbali na mikutano ya kampeni ili kuepuka mgongano.

Wale wote ambao walioonekana kutoridhika na kipindi cha mpito wanataka utawala urejeshwe haraka mikononi mwa raia na kuwaondoa wajumbe wote wa utawala wa serikali ya zamani walio katika sekta mbalimbali na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliojihusisha na vitendo vya rushwa na kutoa dhamana kuhusu mageuzi ya kidemokrasia, wakati nchi sasa inaongozwa na jopo la majenerali la  Baraza Kuu la vikosi vya jeshi (AFSC).

Wakati huohuo, mahakama ya Misri ilitangaza Jumanne Mei 24 kuahirisha kesi ya Rais Mubarak na wanae wawili wa kiume, Gamal na Alaa, ikiwa ni pendekezo lililotolewa na waandaaji  wa maadamano, lakini hata hivyo hakuna tarehe iliotangazwa ya kusikiliza tena kesi hiyo. Wakati ambapo uchaguzi wa bunge umepangwa kufanyika septemba mwaka huu. Wanaharakati wamefahamisha kuwa chama kimoja pekee cha Muslim Brodherhood ndicho kilicho tayari kushiriki uchaguzi huo. Kurekebisha kalenda ya uchaguzi ni moja kati ya maombi ya waandamanaji wanao andamana leo hii nchini Misri.

 

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.